Bodi ya Wadhamini CUF yagoma kusikiliza msimamo wa Jaji Mutungi
Bodi ya Wadhamini ya chama cha Wananchi (CUF) imefanya kikao chake Oktoba 2, 2016 katika Makao Makuu ya Chama hicho mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake, Abdallah Said Khatau ili kujadili wito wa Profesa Ibrahim Lipumba wa kukutana leo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili msimamo na ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuhusu mgogoro unaoendelea ndani ya chama hicho.
Baada ya kikao hicho kufanyika, jana bodi hiyo imetoa tamko lake juu wa wito huo.
Wakati akisoma tamko hilo, Khatau alisema wajumbe wa bodi ya wadhamini wameupuuza wito wa Lipumba.
“Bodi imepuuza wito wa mtu anayeitwa Lipumba alioutangaza juzi kwamba eti amemtaka mtu mwengine anayeitwa Thomas Malima kuitisha kikao cha Bodi ya Wadhamini. Lipumba kwa sasa si Mwenyekiti tena wa CUF na pia si mwanachama wa CUF baada ya kufukuzwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa,” alisema.
Khatau alisema bodi hiyo itaendelea kuwajibika kwa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF kama inavyotakiwa na Ibara ya 98(5), ambalo ndilo linaloiteua bodi na kwamba litaheshimu maamuzi yake yote kwa kuwa ndiyo chombo chenye dhamana ya kusimamia uongozi na uendeshaji wa CUF.
Licha ya kugoma kuitikia wito huo wa Lipumba, Khatau alisema bodi
Itachukua hatua za kisheria chini ya uwezo wake iliopewa na Ibara ya 98(3) na 98(4) ya katiba ya CUF kurejesha chini ya dhamana yake mali zote za Chama alizodai zilivamiwa, kuporwa na kuhodhiwa na Lipumba na genge lake ikiwemo jengo la Ofisi Kuu ya Chama iliopo Buguruni, Dar es Salaam.
“Pia itachukua hatua za kisheria chini ya uwezo wake iliopewa na Ibara ya 98(4) dhidi ya Ibrahim Lipumba kumtaka alipe gharama na hasara zote alizozisababisha kwa kuvamia Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa Chama, tarehe 21 Agosti, 2016 katika Ukumbi wa Blue Pearl, Ubungo Plaza na genge lake kufanya vurugu, ghasia na uharibifu wa mali za hoteli na hatimaye kuvuruga Mkutano Mkuu jambo lililosababisha hasara ya takriban Sh. 600 milioni; na kisha kuvamia Ofisi Kuu ya Chama, Buguruni, Dar es Salaam, tarehe 24 Septemba, 2016 ambapo alisababisha hasara ya takriban Sh. 50 milioni,” alisema.
Aidha, alisema bodi ya wadhamini inawahakikishia wanachama wote wa CUF wa Tanzania Bara na Zanzibar kwamba Bodi yao ya Wadhamini iko makini na itasimama pamoja nao kulinda mali zote za Chama hicho.
0 comments:
Post a Comment