Wafanyabiashara wawili raia wa China, Su Ning (39) na Feng Guang Quan (51) wamepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka matatu ya kusafirisha Sh30 milioni kwenda nchini China, bila kibali cha Gavana wa Tanzania.
Washtakiwa hao wanadaiwa kusafirisha noti za shilingi miatanomiatano 60,000 kinyume na sheria ya ubadilishaji fedha na kwamba, kiwango hicho kilikuwa kimefungwa kwenye mabunda 40. Kila bunda moja lilikuwa na Sh500,000.
Hata hivyo, washtakiwa hao baada ya kusomewa mashtaka yanayowakabili, walikiri kutenda makosa hayo na Mahakama iliwasomea maelezo ya awali ambayo pia walikiri maelezo hayo, ikiwamo begi lililokuwa na mabunda 40 ya noti yenye thamani ya Sh20 milioni.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha, Wakili wa Serikali, Shadrak Kimaro akisaidiana na Estazia William walidai katika shtaka la kwanza, washtakiwa walitenda kosa hilo kati ya Agosti 15 na Agosti 31, mwaka jana.
Ilidaiwa kuwa washtakiwa walikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), wakisafirisha noti 10,000 za shilingi miatanomiatano kwenda nchini China, zenye thamani ya Sh5 milioni bila kibali cha Gavana wa Tanzania.
Hata hivyo, Hakimu Mkeha aliomba apewe muda ili aweze kujiridhisha kupita maelezo na vielelezo vilivyotolewa kabla ya kutoa uamuzi, kesi hiyo inaendelea leo.
“Kesi hii nimeiona ina vitu vingi kabla ya kufanya uamuzi naomba nipewe muda kupitia vielelezo ili kesho (leo) niweze kutoa uamuzi baada ya kujiridhisha ” alisema.
0 comments:
Post a Comment