
Tangu
juzi usiku habari hiyo ndiyo ilikuwa mjadala kwenye vyombo vya habari,
mitandao na kijamii, ndani ya vyombo vya usafiri na vijiweni. Lakini kwa
upande mwingine zilikuwa ni saa 48 nzito zilizoambatana na vikao
mfululizo, kutenguliwa uteuzi na kuteuliwa kwa mkurugenzi mpya.
Alhamisi iliyopita, Dk Malecela alitoa tamko la kuwepo kwa ugonjwa huo.
“Sampuli
za damu kutoka watu 533 zilipimwa. Kati yao, watoto wachanga 80
walizaliwa na ulemavu wa viungo mbalimbali. Kati ya watu 533 waliopimwa,
83 sawa na asilimia 15.6 wamegundulika kuwa wameambukizwa virusi vya
zika,” alisema Dk Malecela.
Siku
iliyofuata, mtaalamu huyo wa tafiti za magonjwa yanayosambazwa na
wadudu, akiambatana na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, aliongea na
waandishi wa habari kurekebisha taarifa yake, akisema alinukuliwa
vibaya.
Suala
hilo liliibua maswali kwa wadau, ambao baadhi wameitaka Serikali
itayarishe utafiti mwingine ili ueleze ukweli kama ugonjwa huo upo
nchini.
Pia,
waliishauri Serikali kutoa elimu itakayowasaidia Watanzania kujua
ugonjwa huo unavyoambukizwa na jinsi ya kujikinga badala ya kusubiri
utafiti.
Zika
ni ugonjwa unaoenezwa na mbu aina ya aedes anayeuma mchana na
husababisha vipele, udhaifu wa misuli na kwa wajawazito husababisha
wazae watoto wenye kichwa kidogo na ubongo mdogo.
Akizungumzia
suala hilo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Jimson Sanga
alisema kinachotakiwa kwa sasa ni kufanyika kwa utafiti mwingine
utakaoleta majibu halisi ya kuwapo au kutokuwapo kwa ugonjwa huo.
Alisema
matokeo halisi ya utafiti huo yatasaidia kuiondolea jamii wasiwasi
walioupata baada ya NIMR kutangaza utafiti wake na baadaye wakaukanusha.
“Nashauri
zifanyike tafiti nyingine ili kuondoa wasiwasi kwa majibu
yaliyokwishatangazwa. Hata kama yatakanusha, tayari vyombo vya habari
vimeshayafikisha mbali na dunia inajua Tanzania kuna zika. Ni utafiti tu
unaweza kusaidia kwa sasa,” alisema.
Sanga
alisema mgongano uliojitokeza baina ya NIMR na Wizara ya Afya,
unatokana na pande hizo mbili kutoshirikishana katika hatua za utafiti,
hadi matokeo yalipotangazwa.
“Kila
taaluma inayo maadili yake, likiwamo suala la utafiti, kKwenye suala
zito kama hili ambalo dunia inalitazama, ingependeza kama kungekuwa na
umakini zaidi, ili kuondoa mkanganyiko uliojitokeza hivi,” alisema.
Kuhusu
hatua zilizochukuliwa na Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa Dk
Malecela, Sanga alisema kwa kuwa tatizo ni namna taarifa zilivyotangazwa
bila wizara husika kujua na si utafiti, ni sawa kuwajibishwa wakati
majibu sahihi yakitafutwa.
Mtafiti
na mtaalamu wa masuala ya kilimo, Dk Aloyce Kulaya alisema suala la
utafiti ni la kitaalamu na kisomi na yeyote anayefanya utafiti anapaswa
kujiridhisha kabla ya kuamua kuutangaza.
Hata
hivyo, alisema baada ya kazi ya utafiti kufanywa na kutangazwa,
haipaswi mtu yeyote kuibuka na kuupinga iwe kisiasa au kwa njia nyingine
yoyote na badala yake utafiti hupingwa kwa utafiti mwingine.
“Ninavyoelewa
mimi, haipaswi kwa mtu au taasisi kufanya utafiti wake mara moja,
utafiti unapaswa kurudia zaidi ya mara moja ndipo uweke hadharani na mtu
anapokuwa hakubaliani nao anapaswa kuujibu kwa utafiti,” alisema Dk
Kikuya.
Alisema
ni vyema kwa watafiti wanapofanya kazi zao, hususan zile zinazohusu
masuala muhimu na yanayoigusa jamii, kuwa makini na kujiridhisha kabla
ya kutoa matokeo hadharani.
Mtafiti
mwingine aliyebobea kwenye masuala ya kisaikolojia, Frank John pia
alisema ni wakati ambao Serikali inapaswa kufanya utafiti mwingine na
kutoa majibu yatakayomaliza malumbano yaliyopo.
Akizungumzia
nafasi ya wasomi katika kuishauri Serikali, Profesa Kitila Mkumbo wa
Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu cha Dar es Salaam, Kitila Mkumbo alisema
kusimamishwa kazi kwa Dk Malecela ni pigo kwa uhuru wa wanataaluma na
wasomi.
“Je,
Serikali itafungia pia journal (jarida) iliyochapisha utafiti huu? Ni
pigo kiasi gani kwa taaluma na uhuru wa wasomi?” alihoji Profesa Kitila
katika akaunti yake ya mtandao wa Twitter.
Alipoulizwa
kwa njia ya simu, Profesa Kitila alikiri kuandika hivyo na kusisitiza
kuwa Serikali ilipaswa kushauriana na NIMR kuliko kumwondoa Dk Malecela.
“Haiwezekani
kulifuta lile chapisho. Matokeo yake yameshachapishwa, hayawezekani
kufutwa, labda kama kuna kasoro za kitaaluma. Andiko hilo linaonyesha
lilishawasilishwa kwenye mkutano wa wanasayansi likakubalika, kwa hiyo
wananchi wanaweza kulipitia wakitaka,” alisema Profesa Kitila.
Alisema Wizara ya Afya ilitakiwa kukutana na uongozi wa NIMR ili kushauriana, kuliko hatua hiyo.
“Walichofanya Wizara ya Afya si sahihi kwa sababu Dk Malecela ameeleza matokeo ya utafiti, wangewasiliana na uongozi wa NIMR.
“Kuna
utafiti uliotolewa na Benki ya Dunia ulioonyesha kuwa nusu ya
wafanyakazi wa sekta ya afya hawana uwezo wa kutibu wagonjwa, ulitolewa
bila kumshirikisha Waziri wa Afya. Mbona hawakulalamika?” alihoji na
kuongeza:
“Hata
sheria za utumishi bado hazijavunjwa kwa sababu Dk Malecela alikuwa
anawasilisha matokeo ya utafiti siyo taarifa ya ugonjwa.”
Taaluma imedhalilishwa
Katika
hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji alisema
uamuzi wa kumtimua Dk Malecela umeidhalilisha taalama nyeti ya afya
nchini.
Dk
Mashinji ambaye ni mtaalamu wa afya ya binadamu, alitoa kauli hiyo jana
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Iringa katika ziara
ya wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema katika Kanda ya Nyasa kukagua uhai
wa chama na kufanya uchaguzi wa kanda.
Dk
Mashinji alitoa wito kwa wataalamu wote nchini kuungana kupinga vitendo
vinavyokiuka na kukandamiza ustawi wa taifa, huku akiwataka kutotoa
ushirikiano kwa Mkurugenzi Mkuu mpya wa NIMR, Profesa Yunus Mgaya.
WHO yanena
Shirika la Afya la Kimataifa (WHO) limesema halina taarifa za kuwepo dalili wala mgonjwa wa zika Tanzania.
Mwakilishi
wa shirika hilo, Dk Grace Saguti alikuwa akijibu swali kama shirika
hilo hupata taarifa za magonjwa mbalimbali ya mlipuko kutoka Wizara ya
Afya.
“WHO
inafanya kazi na Wizara ya Afya kufuatilia taarifa za magonjwa kila
siku katika maeneo yote ya afya, na taarifa huletwa wizarani kisha
tunashirikishwa ili kutoa katika tovuti yetu. Ninachoweza kusema
hatujapata taarifa za magonjwa ambazo zinazoonyesha dalili za mgonjwa
yoyote mwenye zika Tanzania,” alisema Dk Saguti.
Mganga
Mkuu wa Serikali, Mohamed Kambi alisema Wizara ya Afya ina mfumo wa
kupata taarifa kuhusu magonjwa na kupitia mfumo huo hazijapatikana
taarifa za kuwapo wa mgonjwa wa zika.
Kambi
aliwasihi wanataaluma, watafiti na wanasayansi wakitaka kutoa taarifa
zozote kujihakikishia usahihi wa taarifa hizo kabla ya kuzitoa.
Imeandikwa na Elias Msuya, Tumaini Msowoya, Geofrey Nyang’oro, Muyonga Jumanne na Joyce Mmasi wa Mwananchi
0 comments:
Post a Comment