KUNA
vita ya maneno kati ya makundi mawili ya mashabiki wa Muziki wa Bongo
Fleva, wanaowashabikia wasanii Alikiba na Nasibu Abdul ‘Diamond’, kila
upande ukidai mtu wao ndiye anajua zaidi kuliko mwingine.
Ni
mjadala mpana katika mitandao ya kijamii, mitaani na hata miongoni mwa
wasanii wenyewe ambao kwa kificho au waziwazi, wamewahi kuzungumzia nani
mkali katika wawili hao ambao wote ni vijana wenye asili ya Kigoma.
Alikiba
ama King Kiba, ndiye wa kwanza kuingia na kupata jina katika Muziki wa
Bongo Fleva, katikati ya miaka ya 2000 akiwa na singo yake ya kwanza,
Cinderella ndiyo ilimfungulia milango, kwani alichomoza hadi juu ambako
alidumu kwa muda mrefu.
Huenda
Diamond amewahi kuimba kwa kuiga baadhi ya nyimbo za Alikiba, kwa
sababu yeye alianza kupata jina mwaka 2009, mwaka ambao mwenzake tayari
alishakuwa na albamu mtaani.
Unapotaka
kufanya ulinganisho wa wawili hawa ni lazima uchague unataka
kuwalinganisha nini, vinginevyo unaweza kujikuta umewekeza katika chuki
au ushabiki, kitu ambacho hakitakiwi. Kwa mfano, vigumu kupata idadi
kamili ya mashabiki wa wasanii hao, ingawa mapokeo ya kazi zao yanaweza
kumuongoza mtu kuelewa.
Kitu
kimoja cha msingi ambacho wengi wanakubaliana ni kwamba Alikiba ana
uwezo mkubwa wa kuimba na mwenye sauti nzuri kuliko Diamond. Msanii
mmoja chipukizi, Ibrahim Kidugu ‘Wizzy Rapper’ katika kibao chake cha
Kote Nisikike, kwenye mojawapo ya vesi anasema “Ali ni mwanamuziki,
Nasibu Mfanyabiashara.”
Maana
ya Wizzy Rapper ni kuwa Diamond anafanya biashara ya muziki, ndiyo
maana anaonekana kuwa juu ya Alikiba ambaye anafanya muziki kwa mazoea.
Katika
ubora wake, Alikiba aliwahi kukutana na mkali wa R&B duniani, R
Kelly, katika projekti iliyoitwa One8, ambapo wakali nane wa Afrika
walifanya ngoma moja iliyoitwa Hands Across Africa ambao walikuwa ni
yeye, Fally Ipupa, 2Face, Amani, Movaizhaleine, 4X4, Navio na JK.
Licha
ya Kiba kufika nyumbani kwa R Kelly, studio kwake, alishindwa kutumia
ushawishi wa msanii huyo mkubwa ili aweze kumsaidia kuingia katika soko
la Marekani. Mbaya zaidi, alishindwa pia kujitangaza kimataifa kupitia
Fally Ipupa na 2Face ambao ni maarufu kuliko yeye.
Ambwene
Yessaya ‘AY’ alimkutanisha Diamond na Davido wa Nigeria na akafanya
naye Ngoma ya Number One Remix. Hapa kijana yule wa Tandale hakutaka
kuishia kwa msanii huyo pekee, akaingia nchini humo na kufanya kazi na
wasanii karibu wote wakubwa, wakiwemo waliofanikiwa zaidi, P Square.
Hiyo
imempa Diamond kujulikana zaidi na kumfanya kuwa mmoja wa wasanii
wakubwa Afrika, kiasi cha wengi kuhitaji kolabo naye kutoka Afrika
Kusini, Zimbabwe, Ivory Coast na kwingineko Afrika.
Alikiba
haonekani kuwekeza akili yake yote katika muziki anaoufanya. Ni kama
mtu ambaye anafanya muziki kwa kujifurahisha na siyo kufikia malengo
ambayo mashabiki wake wangependa aende. Ana uwezo mkubwa nyuma ya Mic,
lakini ameshindwa kuutumia ili kuliteka soko.
Kiba
anaridhika au labda niseme, mvivu. Katika uhalisia ni makosa
kumshindanisha na Diamond kwa sababu haoneshi kama ni mshindani wake.
Alipokuwa katika ziara yake Ulaya, akaitumia nafasi adimu aliyoipata
kukutana na marehemu Papa Wemba na kufanya naye wimbo.
Baada
ya kuliweza soko la Afrika, Diamond anaonekana wazi kulitamani la Ulaya
na Marekani na hii ndiyo sababu ya yeye kuwa msanii anayelipwa zaidi
kuliko wote kwa sasa hapa Bongo.
Kiba
hatafuti kolabo na watu wa nje kwa vile anadhani ataonekana anamuiga
mwenzake, wakati katika maisha, kuiga vitu vizuri na vya maendeleo ni
jambo la kupongezwa.
Hata hivyo, Kiba anayo nafasi ya kubadilika ili aweze kuwa mshindani wa kweli wa Diamond, vinginevyo asahau.
0 comments:
Post a Comment