CUBA KUISAIDIA ZANZIBAR KATIKA SEKTA YA AFYA


Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Cuba Bwana Salvador Antonio Valdes Mesa wa Tatu upande wa Kushoto na ujumbe wake akizungumza na mwenyeji wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wa kwanza kulia ofisini kwa Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif akimuonyesha mgeni wake Bwana Salvador baadhi ya vitu vya utamaduni kama kanga pamoja na vyakula vya viungo alivyomuandalia kama zawadi ya uwepo wake Visiwani Zanzibar.
Balozi Seif akimkabidhi zawadi ya Kasha Makamu wa Rais wa Cuba Bwana Salvador likisheheni vuti vya utamaduni na vyakula vya viungo mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.
Balozi Seif wa Nne kutoka Kulia na Mgeni wake Bwana Salvador wanne kutoka kushoto wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine walioshiriki kwenye mazungumzo yao ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kulia akimuaga mgeni wake Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Cuba Bwana Salvador Antonio Valdes Mesa mara baada ya mazungumzo yao. Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Cuba Bwana Salvador Antonio Valdes Mesa ameahidi kwamba Nchi yake itaongeza nguvu za uhusiano na Jamuhuri ya Muungano wa Tanazania ili kizazi kipya kipate fursa pana ya kurithi Historia ya muda mrefu iliyopo ya pande hizo mbili.

Alisema anafarajika kuona Sekta ya Afya imepanua zaidi mafungamano ya pande hizo mbili kufuatia kundi kubwa la Madaktari wazalendo kumaliza mafunzo yao ya muda mrefu chini ya usimamizi wa Wataalamu wa Cuba.

Bwama Salvardo Antonio Valdes Mesa alieleza hayo wakati wa mazungumzo yake na Mwenyeji wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwa Balozi Seif Vuga akiuongoza Ujumbe wa Viongozi kadhaa katika ziara yake ya siku mbili Visiwani Zanzibar.

Bwana Salvardo alisema kundi hilo la Madaktari wazalendo waliopata mafunzo hayo litasaidia kuongeza kasi za utoaji wa huduma za Afya kwa Wananchi katika maeneo mbali mbali kama azma na matarajio ya Zanzibar yalivyokusidiwa.



Katika kuimarisha uhusiano huo wa pande hizo mbili za Cuba na Tanzania ikiwemo Zanzibar Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Cuba alieleza kwamba Nchi hiyo itaongeza nafasi za masomo ya juu nay a muda mfupi kwa Wanafunzi wa Zanzibar.

Akigusia Sekta ya Uvuvi wa Bahari Kuu Bwana Salvardor alisema ipo haja ya kuundwa kwa Kamati ya pamoja ya Wataalamu katika Sekta hiyo ili kubadilishana mawazo na utaalamu utakaosaidia kuimarisha mbinu za kukuza Sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa pande hizo mbili.

Alisema mazingira ya Cuba na Zanzibar yanafanana kutokana na nchi hizo mbili kuzunguukwa na bahari hali ambayo iwapo uvuvi wa bahari kuu utaendelezwa unaweza kwa kisi kikubwa kuinua mapato ya Taifa sambamba na Wavuvi wenyewe.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar na Cuba bado zina nafasi kubwa ya kuendelea kushirikiana kutokana na historia ndefu ya uhusiano uliopo baina ya pande hizo mbili.

Balozi Seif aliishukuru Jamuhuri ya Cuba kwa msaada mkubwa iliyotoa katika kuimarisha sekta ya Afya ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kujiimarisha katika kujenga miundombinu imara ya Hospitali na Vifaa.

Alisema Zanzibar bado inahitaji msaada wa madaktari kutokana na ongezeko la ujenzi wa Hospitali za rufaa akazitolea mfano ile ya Abdulla Mzee iliyopo Mkoani Pemba na Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar.

Akigusia sekta ya Viwanda na Uvuvi wa Bahari Kuu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishauri Cuba kupitia kwa Makamu wa Rais wa Nchi hiyo kuangia uwezekano kwa wawekezaji na wataalamu wa Nchi hiyo kuanzisha miradi yao ili kusaidia kupanua soko la ajira sambamba na kuongeza pato la Taifa.

Alifahamisha kwamba Cuba ina wataamau wa kutosha katika sekta hiyo kiasi kwamba wanaweza kusaidia Taaluma katika kuimarisha miundombinu kwenye rasilmali kubwa iliyopo Tanzania ikiwemo Zanzibar .

Bwana Salvardor yuko Nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku 3 yenye lengo la kuimarisha uhusiano kati ya Jamuhuri ya Cuba na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta tofauti kama afya, Elimu, Utamaduni ,Michezo, teknolojia na kuangalia maeneo mengine mapya ya uwekezaji.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Share on Google Plus

About Unknown

Unaweza kuwasiliana nasi kupitia; Email: Epyanastephene@gmail.com Phone:0719337774

0 comments:

Post a Comment