Mwanasiasa wa Kenya alaumiwa kwa marufuku ya miraa Somalia

Wafanyibiashara wa miraa

Sababu kuu ya Somalia kupiga marufuku ndege za kubeba miraa kutoka Kenya kutoingia nchini humo wiki hii ni kwamba imekasirishwa na ziara ya mwanasiasa wa Kenya katika jamhuri iliojitangaza ya Somaliland, kulingana na gazeti la Nation nchini Kenya.

Serikali ya Somalia inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa haitambui Somaliland na kwamba ingetaka jimbo hilo lililojitenga kuungana na Somalia.
Gavana wa kaunti ya Meru nchini Kenya ambapo ndio eneo linalokuzwa miraa alielekea Somaliland mnamo mwezi Julai kuona iwapo anaweza kufanya makubaliano ya kibishara ya miraa.
Peter Munya aliwataka wanunuzi wa miraa ya Ethiopia katika eneo hilo kununua miraa inayotoka nchini Kenya.
Somaliland pia inawatoza kodi kubwa wauzaji wa zao hilo kutoka Kenya.
Hivyobasi serikai ya Somalia iliona ziara hiyo kama kuingilia kati maswala ya ndani ya taifa hilo kulingana na ripoti za gazeti la Daily Nation.
Balozi wa Somalia nchini Kenya ,Gamal Hassan aliliambia gazeti hilo kwamba ziara ya bwana Munya ilisababisha shinikizo ya kisiasa nchini Somalia.
Taifa la Somalia lilianza kutekeleza marufuku hiyo siku ya Jumanne bila maelezo ya kwani nini na kwa muda gani marufuku hiyo itatekelezwa.
Bwana Hassan alisema kuwa serikali yake ilikuwa ikijadili swala hilo na mamlaka ya Kenya ili kutafuta suluhu ya kudumu.
Kulingana na gazeti hilo,Kenya hutuma takriban ndege 540 zilizojaa miraa nchini Somalia kila mwezi.
Marafuku hiyo inaweza kusababisha hasara ya mamilioni ya dola ,hususan wakati huu ambapo Somalia ndio soko kubwa la miraa kutoka Kenya kufuatia marufuku ya zao hilo barani Ulaya,Marekani na Canada.
Kulingana na wale wanaopinga miraa nchini Somalia,ndege za mizigo zinazotua mjini Mogadishu kila siku hupeleka takriban mabagi 12,000 ya miraa yenye thamani ya dola 400,000.
Share on Google Plus

About Unknown

Unaweza kuwasiliana nasi kupitia; Email: Epyanastephene@gmail.com Phone:0719337774

0 comments:

Post a Comment