Na Mwandishi Maalum, New York
Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali, jana ( jumatatu) wamepitish tamko la kwanza la aina yake linalolenga pamoja na mambo mengine kuichagiza jumuiya ya kimataifa kushirikiana katika kukabili wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji.
Kupitia Tamko hilo ambalo linatambulika kama Tamko la New York, linazitaka serikali za mataifa yote, bila kuingilia uhuru wa mambo yao kama mataifa huru au ukiukwaji wa sheria za kimataifa, kuwapokea, kuwahifadhi na kuwapatia huduma za kijamii wakimbizi na wahamiaji bila ya kujali hadhi zao.
Ni tamko ambalo limetokana na majadiliano ya muda mrefu baina ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, Asasi za kiraia na Mashirika ya Kimataifa, majadiliano ambayo wakati mwingine ililazimu wajumbe kukubaliana kutokukubaliana katika baadhi ya vipengele vya tamko hilo.
Upitishwaji wa Tamko hilo la New York kuhusu wakimbizi na wahamiaji umefanyika ikiwa na sehemu ya uliokuwa mkutano wa siku moja uliojadili changamoto kuhusu wakimbizi na wahamiaji ambao idadi yao imezidi kuongeza na kubwa kuwahi kutokea.
Kwa mfano, takwimu zinaoonyesha kwamba, mwaka 2015 idadi ya wakimbizi na wahamiaji ilifikia watu milioni 224, ongezeko ambalo kasi yake ni kubwa kuliko ongezeko la idadi ya watu duniani.
Hata hivyo inaelezwa pia kwamba kuna takribani watu 65 milioni ambao wamelazimishwa kuhama, wakiwamo zaidi ya wakimbizi milioni 21, milioni tatu wanaotafuta hifadhi na zaidi ya milioni 40 wakiwa ni wakimbizi wa ndani.
Wakuu wa Nchi na Serikali pamoja na wakuu wa Mashirika na Taasisi za Kimataifa, wanaahidi kupitia tamko hilo la New York , pamoja na mambo mengine, kulinda haki za binadamu za wakimbizi na wahamiaji wote bila ya kujali hadhi yao. Ikiwa ni pamoja na haki za wanawake na wasichana pamoja na kukuza fursa yao ya kushiriki kikamilifu katika kutafuta suluhu.
Wameahidi pia kuzuia vitendo vya ukatili wa kingono na udhalilishaji dhidi ya wanawake. kuhakikisha kwamba watoto wakimbizi na wahamiaji wanapata elimu mara tu wanapofika nchi ya ugenini.
Vile vile tamko hilo, linashauri na kupendekeza nchi ambazo zimekuwa ama zikipokea wakimbizi na kuwahifadhi au zile ambazo ni njia wanayopitia kwenda nchi nyingine basi zisaidiwe katika ubebaji wa jukumu hilo.
Tamko hilo pia linataka kukomeshwa kwa tabia ya kuwaweka vizuizini watoto ili kubaini hadhi yao ya uhamiaji. Linataka pia kutafutiwa makazi wakimbizi wote ambao wanatambuliwa na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi kuwa wanaohitaji makazi, pamoja na kuwatafutia fursa za kuhamia nchi nyingine.
Katika kuhakikisha changamoto ya wakimbizi na wahamiaji linashughulikiwa katika ukamilifu wake, Umoja wa Mataifa umeamua katika mkutano huo wa Jumatatu kuiingiza rasmi Shirika la Kimataifa la Wahamiaji ( IOM) kuwa chini ya mfumo wa Umoja wa Mataifa.
Wakati huo huo, Rais wa Marekani, Barack Obama, ameeitisha siku ya jumatano Mkutano wa Viongozi kuhusu Wakimbizi. ( Leaders’ Summit on Refugees) . Katika mkutano huo viongozi wakuu wa nchi na serikali walioalikwa watatarajiwa kutoa ahadi zao kuhusu namna serikali zao zitakavyo wasaidia wakimbizi.
Tanzania ni kati ya nchi zilizoalikwa kuhudhuria na kushiriki mkutano huo. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Augustin Mahiga ( Mb) anayeongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Anatarajiwa kuwasilisha ahadi ya Tanzania katika Mkutano huo.
0 comments:
Post a Comment