LIGI YA MABINGWA ULAYA ARSENAL CHALI MBELE YA BARCELONA, JUVENTUS YASALIMU AMRI KWA BAYERN MUNICH

Wakicheza ugenini katika uwanja wa Camp Nou, washika bunduki wa jiji la London usiku wa kuamkia leo walijikuta wakiondolewa katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya baada ya kukubali kichapo cha mabo 3-1. 

Arsenal ambao katika mchezo wa awali uliochezwa katika uwanja wao wa nyumbani walikubali kipigo cha mabao 2-0, pia jana usiku walijikuta wakiwa na wakati mgumu mbele ya FC Barcelona.
Ulikuwa ni muunganiko wa wadunguaji mahiri wa FC Barcelona, MNS, ambao ni Messi, Neymar na mtukutu mstaafu Suarez. 

Katika mchezo huo ambao uliendelea kumuweka katika wakati mgumu kocha mkuu wa Arsenal, Arsene Wenger, mchezaji Neymar ndiye aliyekuwa wa kwanza kuifungia timu yake bao katika dakika ya 18. 

Kipindi cha pili cha mchezo huo Luis Suarez akafunga bao la pili katika dakika ya 65 kabla ya Lionel Messi kukamilisha idadi ya mabao kwa kufunga bao la tatu katika dakika ya 8. 

Bao pekee la washika bunduki wa London lilifungwa na Mohamed Elneny katika dakika ya 51. Kwa matokeo hayo Barcelona imesonga mbele hatua ya robo fainali kwa jumla ya mabao 5-1
DUH HAWA WATU GANI HAWANA HURUMA!! Wachezaji wa Arsenal wakiwa hawaamini kipigo walichopata kutoka kwa wenyeji wao FC Barcelona
Katika mchezo mwingine wa ligi ya mabingwa barani Ulaya uliochezwa usiku wa kuamkia leo, Bayern Munich wakicheza nyumbani katika uwanja wa Allianz Arena wameibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Juventus kutoka Italia.

Hata hivyo nusura mashabiki wa Bayern wahisi jahazi linazama nyumbani kwao baada ya kushuhudia timu yao ikifungwa mabao mawili ya haraka haraka ndani ya kipindi cha kwanza.
Alikuwa ni Paul Pogba aliyeanza kuifungia Juventus bao la kwanza kunako dakika ya 5 ya mchezo kabla ya Juan Cuadrado kufunga bao la pili katika dakika ya 27. Mabao hayo yalidumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika huku Bayern wakiwa hawana kitu.

Kipindi cha pili kilikuwa kichungu kwa Juventus, kwani walishuhudia wakifungwa mabao manne na kuondolewa katika michuano hiyo. 

Mabao hayo ya Bayern yaliwekwa kimiani na wachezaji Robert Lewandowksi katika dakika ya 72, Thomas Muller akifunga bao la pili katika dakika ya 90, Thiago Alcantara akafunga bao la tatu katika dakika ya 106 na bao la nne nala ushindi likafungwa na Coman katika dakika ya 109. 

Kwa matokeo hayo, Bayern Munich imechomoza hatua ya robo fainali kwa jumla ya mabao 6-4.




Share on Google Plus

About Unknown

Unaweza kuwasiliana nasi kupitia; Email: Epyanastephene@gmail.com Phone:0719337774

0 comments:

Post a Comment