Siri
ya utoroshaji wa wanyama na wadudu hai kutoka Tanzania kwenda nje ya
nchi imebainika. Wamekuwa wakitumika katika nchi mbalimbali kwenye
utafiti, mapambo na kitoweo.
Uchunguzi
uliofanywa na waandishi wetu, umebaini matumizi hayo na kuwa wanyama
wanaotakiwa kwa wingi ni mijusi ya bluu, kenge na tumbili wanaopelekwa
katika nchi za Ulaya kupitia viwanja viwili vya ndege hapa nchini.
Mkurugenzi
wa Idara ya Wanyamapori, Herman Keraryo alisema mbali na wanyama hao,
wengine wanaopelekwa nje ni jamii ya nyani, wadudu na ndege.
Alisema hakuna nchi ambayo imejitambulisha kipeke kununua wanyama hao, bali imekuwa ni biashara kati ya mzawa na mnunuzi.
Alipoulizwa
kuhusu uhalali wa biashara hiyo, Keraryo alisema mfanyabiashara lazima
awe na leseni inayotambuliwa na Serikali; “... na siyo kila ndege
anasafirishwa au nyani, kuna aina ya ndege wasioruhusiwa ila kwa
kutozingatia sheria, baadhi ya watu wanaivunja.” Mkurugenzi Mkuu wa
zamani wa Tanapa, Gerald Bigurube alisema wanyama kama kobe na kakakuona
nao wamekuwa wakisafirishwa zaidi kwenda Vietinam na China kwa matumizi
ya chakula na dawa.
Alisema matumizi mengine ya wanyama hao wanaopelekwa Marekani na Ulaya yamekuwa ni kwa ajili ya shughuli za mapambo.
“Wanyama
hai na wadudu kwa kifupi wana soko pana sana duniani na matumizi yake
ni kama hayo lakini inakuwa vigumu kujua moja kwa moja wanapelekwa nchi
gani,” alisema.
Bigurube
alisema wanyama wengine wamekuwa wakipelekwa kwenye maeneo ya mafunzo
ili watu wengine duniani wajifunze historia yao. Imeelezwa kuwa mijusi
ya bluu ambayo inapatikana Tanzania pekee ndiyo inayotafutwa zaidi na
kila mmoja umekuwa ukiuzwa kwa Euro 5,000 (Sh12.2 milioni.)
Kwa
mujibu wa vyanzo mbalimbali ndani ya Idara ya Wanyamapori, wimbi la
ukamataji na utoroshaji wa mijusi hiyo na tumbili linatokana na
kuhitajika katika nchi mbalimbali kwa ajili ya utafiti.
“Kitu
kinachoibwa zaidi sasa hivi nchini ni hao tumbili kwa sababu wanatumika
sana huko nje kwa ajili ya utafiti wa kitabibu,” kilidokeza chanzo
chetu na kuongeza: “Hata unavyoona, faru wanauawa ni kwamba wenzetu huko
nchi za Asia wanaamini unga wake unasaidia kuongeza nguvu za kiume.”
Matumizi
hayo yamebainika siku chache baada ya vyombo vya dola kuwashikilia raia
wawili wa Uholanzi kwa kosa la kusafirisha tumbili 61 ambao walikuwa
wapelekwe Albania kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro
(Kia).
Habari
zilizopatikana juzi zilidai kwamba mmoja wa maofisa wanyamapori alipewa
bakshishi ya Dola 3,000 za Marekani, sawa na Sh6.4 milioni za Tanzania
katika ‘dili’ hiyo ya tumbili 61.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alikiri kuwa tumbili
na mijusi hao wa bluu ndiyo wanaowindwa zaidi kwa sasa; “... na huyo
Williams Blue Lizard ni mjusi anayepatikana Kimboza na Ruvu. Ndiyo
maeneo pekee duniani. Huyo mjusi anakaa juu ya miti kwa hiyo
wanachofanya ni kukata mti na kuuangusha ndipo wanawakamata na kuwaweka
kwenye mabegi. Wanafanya uharibifu mkubwa.”
Profesa Maghembe alisema mijusi hao huuzwa kati ya Euro 5,000 hadi 6,000 kila mmoja katika nchi za Ulaya.
Kuhusu
tumbili, Profesa Maghembe alisema mpango ulikuwa ni kukamata tumbili
441 kwa awamu lakini kikwazo kikubwa kilikuwa ni upatikanaji wa kibali
cha kuwasafirisha kwenda nje.
Alipoulizwa
kwa nini raia hao wa Uholanzi wamekamatwa wakati walikuwa na kibali,
alisema kibali hicho kilitolewa katika mazingira ya rushwa.
“Ni
kweli walikuwa na kibali lakini kilitolewaje wakati nilishazuia na
waraka ukatolewa? Lakini ujue hawakuwa na kibali pia cha kuwakamata hao
wanyama,” alisema.
“Hili
jambo lina njama kubwa na ndiyo maana tumeamua lichunguzwe na kile
kikosi kazi cha kitaifa ambacho huchunguza makosa makubwa ya kihalifu,”
alisisitiza.
0 comments:
Post a Comment