
WAKATI uchaguzi wa marudio ukitarajiwa kufanyika jumapili
visiwani Zanzibar, Chama Cha Wananchi (CUF) kimesema kuwa haki za
binadamu zimeendelea kuminywa kwa kiasi kikubwa visiwani humo huku
wafuasi wa chama hicho wakilengwa zaidi.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara) , Magdalena
Sakaya, ameyasema hayo leo wakati alipozungumza na waandishi wa habari
kwenye Makao Makuu ya Ofisi za Chama hicho zilizopo Buguruni jijini
hapa.
Magdalena amesema kuwa Tanzania imeridhia mikataba
mbalimbali ya kimataifa ya haki za binadamu hivyo mambo yanayotokea
Zanzibar ni ya kushangaza na hayapaswi kufumbiwa macho kwa ustawi wa
Taifa.
Amesema kuwa baada ya CUF kutangaza kujitoa kwenye
kinyang’anyiro cha uchaguzi wa marudio , wananchi wa Zanzibar wamekuwa
wakiishi kwa hofu huku vikundi vya matukio ya uhalifu maarufu’mazombi’
yakipiga watu pasipo na kuchukuliwa hatua zozote na vyombo vya usalama.
“Mara kwa mara tumekuwa tukiwaambia jeshi la polisi
kuhusiana na haya mazombi ila cha kushangaza hadi leo hakuna taarifa
yoyote iliyotolewa kuhusiana na kukamatwa kwa makundi hayo ya mazombi,”alisema.
Chama hicho kimesema kuwa viongozi wao kadhaa wamekamatwa
kwa nyakati tofauti ambapo jana Mkurugenzi wa Habari na Uenezi Taifa
-Hamad Masoud, alikamatwa na kuwekwa kizuizini na Polisi baada ya kutoa
taarifa ya matukio mbalimbali yanayoendelea visiwani humo ambayo ni ya
kinyume na haki za binadamu.
“Jambo la kushangaza kila tukio baya likitokea
wanasingiziwa wafuasi wetu, mara kwa mara wamekuwa wakikamatwa na tangu
januari hadi sasa zaidi ya wafuasi 60 wamekamatwa kwa madai ya kuhusika
na uvunjifu wa amani,”alisema.
“Sisi tumeamua kujitoa kwenye uchaguzi huo ili wananchi wetu wawe huru na kuwaepusha kwenye vurugu, kwa hiyo
Chama cha Mapinduzi kisiwalazishe wananchi kufanya mambo
ambayo wenyewe hawako tayari kuyafanya na kuyaona ni kinyume na Katiba,
kwa sababu uchaguzi huo wa marudio ni haramu.
“Asilazimishwe mbuzi kunywa maji wakati hana kiu,”alisema Magdalena na kuongeza kuwa wangetegemea uchaguzi huo kufanyika kwa amani baada ya kutangaza kujitoa mapema mwaka huu.

Magdalena alisema kuwa yapo maeneo kadhaa visiwani humo
wananchi wamepigwa marufuku ya kutoonekana wakitembea kuanzia saa mbili
usiku hatua inayosababisha hata wengine kushindwa kwenda kufanya ibada.
Akizungumzi kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Charles Kitwanga, ya kusema kuwa hakuna watu wanaopigwa visiwani humo,
Kiongozi huyo wa Chama alipinga madai hayo na kusema kuwa ni hatari
kuudanganya umma kwa kuficha ukweli na kuacha watanzania wateswe.
Aliishauri Serikali kuhakikisha kuwa usalama wa wananchi
visiwani humo unaimarishwa kwa kufuata misngi ya haki za binadamu na
utawala bora, pia ichukue hatua dhidi ya ‘mazombi’ ambayo yamekuwa
yakiripotiwa kupiga watu kwa nyakati tofauti.
About Unknown
Unaweza kuwasiliana nasi kupitia; Email: Epyanastephene@gmail.com
Phone:0719337774
0 comments:
Post a Comment