Magazeti
MWANANCHI
Michango ya kampeni za kujinadi kwa wananchi katika majimbo mbalimbali nchini imelalamikiwa na baadhi ya wanachama wa CCM wanaowania kuteuliwa kugombea ubunge.
Kutokana na ukali wa michango hiyo, baadhi ya wagombea wamelazimika kujitoa katika mchakato, wengine wakisema hawawezi kumudu kulipa fedha hizo kwa maelezo kwamba ni kiwango kikubwa. Michango hiyo inatofautiana baina ya jimbo moja na jingine.
Hata hivyo chama hicho kimesema hakitishwi na wachache wasioridhishwa na uamuzi unaofanywa kwa masilahi mapana ya chama hicho.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema: “Tunaendelea na mchakato wa kura ya maoni. Kila mtu yuko bize na kura, siwezi kuzungumzia watu wachache wasioridhika wakati wengi wanaendelea na utaratibu tuliojiwekea.”
Wagombea watatu katika Jimbo la Bukoba Mjini wamelalamikia kuchangia gharama hizo ambazo kwa mujibu wa agizo la Kamati ya Siasa ya Wilaya, kila mmoja anatakiwa kutoa Sh2 milioni hadi ifikapo leo kabla ya kuanza kwa kura za maoni Agosti Mosi.
Mmoja wa wagombea hao, George Rubaiyuka alidai kuwa kiasi hicho ni kikubwa na kwamba alikuwa tayari amelipa Sh200,000 huku mgombea mwingine, Dk Anatory Amani akiomba aongezewe muda ili akamilishe malipo hayo.
Mgombea mwingine ambaye hajakamilisha malipo hayo ni Mujuni Kataraiya ambaye pia alipendekeza Kamati ya Siasa kuangalia upya kiwango kilichowekwa.
Aliyekuwa mgombea ubunge katika Jimbo la Chalinze, Imani Madega amekaririwa akisema hataweza kukamilisha ndoto yake ya kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo kutokana na gharama kuwa kubwa.
Kadhalika, mgombea ubunge Jimbo la Morogoro Mjini, Simon Berege alisema kikao cha Kamati ya Siasa ya Wilaya kilikutana Julai 21 na kuchanganua gharama za uchaguzi na kila mgombea alitakiwa kulipa Sh6.9 milioni siku hiyohiyo tena zikiwa taslimu.
Berege alisema baada ya uamuzi huo aliomba kupewa muda hadi siku ya pili kukamilisha lakini mgombea mwenzake alijitolea kumkopesha jambo ambalo hakuliafiki.
“Ninaamini ukubwa wa gharama iliyowekwa na sharti la kutokushiriki kwenye kampeni hizo isipokuwa tu kwa kulipa fedha hiyo yote ama kwa awamu mbili na kuzuia mtu kufika kwenye mikutano ya kampeni kwa usafiri binafsi umefanywa kwa makusudi ili kufanikisha nia ile ya awali ya kuwa na mgombea mmoja,” Berege.
Alisema katika mikutano ya kampeni ambayo amekuwa hahudhurii, imekuwa ikitolewa taarifa kuwa amejitoa jambo ambalo si sahihi na kwamba amekuwa akiwasiliana na mkurugenzi wa uchaguzi wa chama akimweleza kuwa anaendelea kufanya jitihada za kutafuta fedha huku akitaka jina lake liendelee kutajwa katika mikutano ya kampeni.
Katibu wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Kulwa Milonge alisema hakuna mizengwe ya aina yoyote inayofanyika na kwamba chama kinamtambua Berege kuwa ni mgombea kwa kuwa fomu yake imejazwa kwa usahihi.
Alisema Berege haonekani katika kampeni za kujitambulisha kwa wanachama na kwamba alipewa muda wa kutafuta fedha zilizotakiwa kwa ajili ya gharama za kampeni hiyo, hawezi kutajwa mpaka atakapoonekana katika kampeni.
MWANANCHI
Waziri mkuu mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim amesema chama chochote cha siasa nchini kina nafasi ya kushika dola endapo kitafuata kanuni na taratibu zilizowekwa na mamlaka husika.
Dk Salim alisema hayo jana baada ya kufungua semina iliyoandaliwa na Taasisi ya Utamaduni na Urithi kutoka Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro (MUM).
Alisema demokrasia katika vyama vya siasa imezidi kukua na kwamba kikubwa kinachotakiwa ni kutumia njia bora na siyo kurushiana maneno ambayo hayana msingi.
“Utakuta viongozi wa vyama wenyewe kwa wenyewe wanarushiana maneno, huyu hafai mara siyo raia wa nchi hii, sasa haya mambo kwenye siasa hayatakiwi.
“Ni lazima kila kiongozi wa chama cha siasa atambue wajibu wake katika jamii,” Dk Salim.
Pia maadili ya viongozi katika Taifa yameporomoka, hivyo aliwaasa wananchi kuchagua viongozi bora kwa masilahi ya Taifa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.
“Sasa kiongozi anagombea nafasi fulani kwa masilahi yake binafsi, siyo kwa wananchi na anawaomba wampigie kura,” Dk Salim.
Aliwataka wananchi kuwa watulivu na kuilinda amani katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Katika semina hiyo ya Urithi na Utamaduni wa Tanzania alisema nchi ina urithi lakini haujapewa kipaumbele pia suala la uchumi na maendeleo ndilo lililopewa kipaumbele.
Hata hivyo, alisema jamii haijachelewa na inaweza kuweka mikakati itakayofanya jambo fulani kutambulika zaidi.
Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Prof. Abdallah Bujra alisema semina hiyo itakuwa ya siku tatu.
MWANANCHI
Katika dakika za mwishomwisho wakati wa mchakato wa kuwania urais kwa tiketi ya CCM, habari za mmoja wa wagombea aliyekuwa na nguvu katika kinyang’anyiro hicho, Edward Lowassa kwamba angeenguliwa zilivuma mno na kuibua swali la atakatwa hakatwi?
Baada ya Kamati Kuu ya chama hicho (CC), kutangaza majina matano ya waliopitishwa katika hatua ya awali, bila ya jina lake kuwamo, likaibuka swali la pili; atatoka hatoki?
Sasa jibu la swali hilo la pili limepatikana. Ametoka na sasa ni rasmi kwamba atakuwa mgombea urais kupitia Ukawa.
Usiku wa kuamkia jana, Waziri Mkuu huyo wa zamani alihudhuria rasmi kikao cha Kamati Kuu ya Chadema katika kile kilichoelezwa kuwa ni kutambulishwa pamoja na kujadiliana mikakati ya kuing’oa CCM madarakani.
Baada ya jana mchana, viongozi wa Ukawa, Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi, James Mbatia; Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba walikutana na waandishi wa habari Dar es Salaam na kumkaribisha rasmi Lowassa kwenye umoja huo huku wakitumia muda mrefu kumsafisha dhidi ya tuhuma mbalimbali ambazo amekuwa akihusishwa nazo.
Mwandishi wetu alimshuhudia mbunge huyo wa Monduli akihudhuria kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya Chadema juzi usiku.
Awali kikao hicho kilianza saa 9.30 alasiri katika Hoteli ya Ledger Bahari Beach, Dar es Salaam ambacho Wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho walipata taarifa ya kufanyika kwa kikao hicho ghafla Jumamosi kati ya saa nne na tano usiku kwa kupigiwa simu, lakini hawakuambiwa ukumbi wala madhumuni ya kikao hicho zaidi ya kuambiwa kuwa wanatakiwa wawepo Dar es Salaam siku hiyo.
Lowassa alialikwa kuhudhuria kikao hicho na aliwasili katika lango la kuingia kwenye hoteli hiyo saa 3.02 usiku akiwa ndani ya gari jeusi aina ya Toyota Lexus, akiwa amevalia suti nyeusi na shati jeupe na kupokewa na viongozi mbalimbali wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe.
Baada ya hapo aliongozwa kuelekea katika Chumba cha Wageni Mashuhuri (VIP) na kukutana na viongozi wachache wa chama hicho wakiwamo Mbowe na Makamu Mwenyekiti (Zanzibar), Said Issa Mohammed.
Mazungumzo hayo yalidumu kwa takribani dakika 18 na ilipofika saa 3.20 usiku, walitoka na kuingia katika ukumbi ambao kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kilikuwa kinafanyika.
Lowassa alishiriki kikao hicho kwa takriban dakika 98 na ilipofika saa 4.58 usiku, alitoka katika ukumbi huo akisindikizwa na Mbowe, Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa, Makamu Mwenyekiti (Bara), Profesa Abdallah Safari, Mohammed na Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu ambao baadaye walirejea ukumbini kuendelea na kikao.
Tofauti na mikutano ya nyuma ya umoja huo, Mbowe jana hakuzungumza chochote licha ya kuulizwa maswali moja kwa moja kuhusu kauli zake za awali zilizowahi kuonekana bayana kumshambulia Lowassa.
Hata alipofuatwa na wanahabari baada ya mkutano huo hakuzungumza chochote zaidi ya kueleza kuwa mambo yote yameelezwa kwa kina na wenzake.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Mohamed alipotakiwa kuthibitisha taarifa za Lowassa kushiriki vikao vya Chadema na kwamba ameshajiunga na chama chao, alisema kwa kifupi: “Sitaki kuzungumzia lolote juu ya hilo.”
NIPASHE
Mbunge wa Viti Maalum, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mkoa wa Mara, Leticia Nyerere, ametangaza rasmi kukihama chama hicho na kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa madai kuwa alikurupuka kuhamia Chadema na kwamba anarudi nyumbani.
Mbunge huyo ambaye aliambata na watoto wake wawili, alieleza msimamo wake kwa waandishi wa habari jana Dar es Salaam.
Alisema awali alikuwa CCM, isipokuwa alikihama chama hicho kutokana na tamaa na kudhani kuwa Chadema kinaweza kumfaa, lakini baada ya kujiunga chako alifanya kazi vizuri ingawa alikosa amani ya moyo.
“Kweli Chadema nilipokelewa vizuri na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, lakini nimegundua kuwa maamuzi yangu hayakuwa sahihi naweza kusema kuwa nilikurupuka na nilidhani nilikokuwa naenda naweza kupata ninachokitamani, lakini baada ya kuingia nimeona bora nirudi nyumbani,” alisema bila kueleza sababu za kutoondoka mapema na kusubiri Bunge livunjwe.
“Mimi ni mwana CCM, ambaye nilianza tangu nikiwa chipukizi na nilisomeshwa Urusi, hivyo nimekaa na kuona kuwa natakiwa kurudi nyumbani ambako kuna wazazi, familia yangu,” Nyerere.
NIPASHE
Mbunge wa Singida Kaskazini aliyemaliza muda wake, Lazaro Nyalandu, amewataka wagombea wenzake kuacha kucheza rafu na kumchafua na badala yake waendeshe siasa safi kwa maendeleo ya wananchi.
Amesema vitendo vya hujuma vinavyofanywa na baadhi ya washindani wake wanaowania ubunge kwenye jimbo hilo kwa kuandaa makundi ya kumzomea, haviwezi kuleta tija kwa wapigakura.
Nyalandu ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema ni muhimu kwa wagombea wote kufuata kanuni na taratibu za uchaguzi ili mwisho wa siku apatikane mgombea bora atakayewasambaratisha wapinzani.
Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za CCM Mkoa wa Singida jana kuhusiana na mchakato wa uchaguzi ndani ya Chama unavyoendelea.
Alisema baadhi ya wagombea wamekuwa wakiacha kueleza sera za mikakati na badala yake kumpaka matope.
Hata hivyo, alisema kamwe hatakata tamaa na badala yake ataendelea kuwafikia wana-CCM na kueleza mikakati yake ya kuwatumikia na kwamba mengi aliyoahidi ameyatekeleza kwa mafanikio makubwa.
“Siasa safi ndiyo zinazotoa na kujenga wagombea makini, bora na wenye ushindani dhidi ya upinzani. Siasa za kuandaa watu wachache ili wamzome Nyalandu, haziwezi kuwa na tija kwa maendeleo ya wananchi wetu,” alisema.
Aliongeza: “Tushindane kwa hoja na mikakati ya maendeleo kwa wapigakura wetu ili mwisho wa siku twende kuwakabili wapinzani tukiwa kamili na wamoja ili kusaka ushindi wa kishindo.”
Alisema kitendo cha kuwashikisha mabango yenye picha zake wanafunzi na kuwapiga picha na kuweka kwenye mitandao, kamwe hakiwezi kumchafua ama kumkatisha tamaa badala yake ataendelea kusonga mbele na kuwa bora zaidi katika kunadi sera zake mbele ya wapigakura.
Kauli hiyo ya Nyalandu imetokana na baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa wapinzani wake, kumzomea na kupiga kelele wakati anapojieleza kwa wananchi kwa lengo la kumvuruga.
Hata hivyo, alisema anafahamu mambo hayo hujitokeza kwenye siasa na bado ana dhamira na uwezo wa kuwatumikia wapigakura wa Singida Kaskazini.
HABARILEO
Serikali imekanusha taarifa ya gazeti la Mwananchi, inayosema kuwa Rais Jakaya Kikwete ni miongoni mwa marais watano wa Afrika wanaolipwa mishahara minono barani Afrika.
Imesema kuwa habari hiyo siyo za kweli, imejaa uongo, uzandiki na uzushi tena wa hatari.
Aidha, imesema mshahara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwezi ama kwa mwaka, haufikii na hata wala kukaribia kiwango kinachotajwa na gazeti la Mwananchi cha dola 192,000 (karibu Sh milioni 400) kwa mwaka, sawa na dola 16,000 kwa mwezi, sawa na Sh milioni 33.2. Dola moja kwa sasa ni sawa na Sh 2,077.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari, si Rais Kikwete tu, bali tangu Uhuru mwaka 1961, Rais wa Tanganyika na baadaye tangu mwaka 1964 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amekuwa miongoni mwa viongozi wanaolipwa mishahara ya chini kabisa duniani.
“Mshahara wa Rais wa Tanzania kwa mwezi ni wa chini kiasi cha kwamba mshahara wake unazidiwa, tena kwa mbali, na mishahara wanayolipwa baadhi ya watendaji wakuu wa baadhi ya taasisi za umma nchini,” ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilikuwa inajibu habari, iliyochapishwa katika toleo lake la jana la gazeti hilo katika Ukurasa wake wa 26, iliyosomeka “Marais watano wanaotajwa kuongoza kwa mishahara minono barani Afrika ni hawa hapa”.
Katika habari hiyo ambayo gazeti hilo, linadai chanzo chake ni “Uchambuzi wa Mtandao wa African Review”, inadaiwa kuwa Rais Kikwete anashikilia nafasi ya tano miongoni mwa viongozi 38 wa nchi za Afrika, wanaolipwa mshahara mnono zaidi.
“Habari hizi siyo za kweli. Ni uongo na uzandiki. Ni uzushi mtupu na ni uzushi wa hatari. Mshahara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwezi ama kwa mwaka haufikii na hata wala kukaribia kabisa kiwango kinachotajwa na gazeti la Mwananchi,” ilisisitiza taarifa hiyo.
Iliongeza kuwa; “Ni jambo la kushangaza kwamba gazeti la Mwananchi, linalochapishwa hapa nchini, linaweza kupata kiasi cha uongo anacholipwa Rais wa Tanzania katika mitandao ya nje badala ya kuuliza rasmi na kupewa majibu sahihi.”
“Kwa kujiingiza katika uzushi wa kupindua kiasi hiki, gazeti la Mwananchi haliwezi kuwa na nia nyingine yoyote isipokuwa nia ya kuwachochea wananchi na kuwajengea chuki dhidi ya Serikali yao na Kiongozi wao Mkuu. “Ni matarajio yetu, kuwa gazeti la Mwananchi litafanya jitihada za makusudi, kama taaluma ya uandishi wa habari inavyoelekeza, kutafuta usahihi wa jambo hili na kuwaambia Watanzania ukweli.”
HABARILEO
Naibu Kamishna Kitengo cha Upelelezi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Loicy Apollo, amekiri kupokea kiasi cha Sh milioni 80.8 kutoka kwa James Rugemalira, na kufafanua kuwa alipatiwa kiasi hicho kama mkopo usio na riba wa matibabu na biashara.
Hata hivyo, alishindwa kuthibitisha kwenda nje kutibiwa na fedha hizo, zaidi ya kukiri kuwa Machi mwaka 2014 alitoa Sh milioni 20 kwa ajili ya kukarabati nyumba yake iliyopo Tarime na kujenga kisima cha maji.
Kamishna huyo alikanusha mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma tuhuma sita zinazomkabili, ikiwemo kuomba na kupokea kiasi hicho cha fedha kutoka kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, ambayo inajihusisha kibiashara kupitia kodi na TRA.
Akijitetea mbele ya baraza hilo, kuhusu tuhuma hizo zinazomkabili, Apollo alisema haelewi amehusishwa vipi kwenye sakata la ufisadi wa akaunti ya Escrow kutokana na ukweli kuwa fedha hizo, alipewa na Rugemalira baada ya kufiwa na mumewe na hali yake kiafya kuwa mbaya.
“Rugemalira nafahamiana naye kwa kuwa alikuwa ni rafiki yake mume wangu, baada ya mume wangu kufariki alionesha kuwa na wasiwasi na afya yangu, ndipo aliponiambia nifungue akaunti ili anitumie fedha za matibabu na zitakazobaki nifanyie biashara, ikiwa kama mkopo usio na riba,” alifafanua.
Alisema tuhuma zinazodai kuwa ameomba na kupokea kiasi hicho cha fedha kwa maslahi yake binafsi kutoka kampuni ya VIP, ni kinyume na Kanuni za Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kuwa kampuni hiyo, ina uhusiano wa kikazi kupitia kodi na TRA anakofanyia kazi.
Aidha, alikanusha madai ya kukiuka kanuni za watumishi wa TRA, zinazowakataza kukopa au kuomba fedha kwa mtu au taasisi yoyote yenye uhusiano wa mamlaka hiyo na kusisitiza kuwa alipokea fedha hizo akiwa kama mtanzania wa kawaida na si mtumishi wa TRA.
“Kwani hata ukiwa nyumbani kama mumeo analipa kodi, hapaswi kukupa mkopo eti kwa sababu wewe ni mtumishi wa TRA? Alihoji Apollo.
Aidha, alisema anachofahamu yeye fedha hizo alipatiwa na Rugemalira na si kampuni ya VIP.
“Hata hivyo, niliieleza tume ya Sekretarieti ya maadili iliponiita kunihoji kuwa nilipokuwa kazini sikuhusika kabisa na tathmini ya kodi ya kampuni ya VIP, idara yangu ni kampuni zilizokwepa kodi, na hii ilishalipa kodi,” alisema.
Kuhusu tuhuma za kushindwa kutamka umiliki wa hoteli yake ya Classic iliyopo Kinondoni kupitia tamko la rasilimali na madeni la mwaka 2012, 2013 na 2014, alikiri kumiliki hoteli hiyo katika miaka ya 2008 hadi 2009 na kusisitiza kuwa kwa sasa hoteli hiyo imeshakufa.
“Sikuweza kutamka kumiliki hoteli hii kwa kuwa ilishakufa tangu mwaka 2009, na hata jengo halikuwa langu, ni la ndugu yangu, kafuatilieni. Mimi nimeanza kutoa tamko la mali na madeni kwa viongozi wa umma mwaka 2010,” alisema.
Awali, shahidi kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Zahara Guga, alidai mbele ya baraza hilo, kuwa Februari 24, mwaka 2014, kupitia akaunti yake namba 0012102684801 iliyoko katika benki ya Mkombozi Tawi la St. Joseph, Appollo alipokea Sh milioni 80.8 kutoka kwa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd.
Aidha, alidai kuwa sekretarieti ya maadili inayo ushahidi wa kutosha kuwa mshitakiwa huyo alikiuka maadili ya viongozi wa umma, kwa kuomba na kupokea kiasi hicho cha fedha akiwa kiongozi wa umma na kusababisha mgongano wa kimaslahi, kwa kuwa VIP ina uhusiano wa kikazi na TRA.
Shitaka la sita halihusiani na miamala ya akaunti ya Escrow, ambapo anadaiwa kuficha taarifa muhimu alizopaswa kuingiza katika matamko yake ya rasilimali na madeni kwa kipindi kilichopo kati ya 31 Desemba 2011 na 31 Desemba 2014, matamko ambayo amekuwa akiyawasilisha kwa Kamishna wa Maadili kwa mujibu wa sheria.
HABARILEO
Serikali imeongeza muda wa mwisho wa kukamilisha ukusanyaji wa takwimu za Sensa ya Viwanda kote nchini hadi Agosti 31 mwaka huu, kutokana na viwanda 366 vilivyoko Dar es Salaam kushindwa kuwasilisha taarifa muhimu za uzalishaji kwenye madodoso ya sensa hiyo.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki alipokuwa anazungumzia kuongezwa kwa muda wa sensa hiyo ya viwanda, akifafanua kuwa viwanda 366 ambayo ni sawa na asilimia 20 katika Jijini Dar es Salaam vimeshindwa kukamilisha na kurudisha madodoso ya taarifa muhimu za viwanda hivyo.
Alisema sensa hiyo ilianza Machi 9 mwaka huu na ilitarajiwa kukamilika Juni 8, 2015, lengo likiwa kukusanya takwimu sahihi zinazohusu Sekta ya Viwanda na mchango wake katika uchumi wa Tanzania.
Sensa hiyo, pamoja na mambo mengine ililenga kupata viashiria sahihi vya uchumi pamoja na taarifa muhimu za viwanda zikiwemo orodha ya viwanda kimkoa, anuani na mahali vilipo, aina ya umiliki na utaifa wa wamiliki.
Takwimu nyingine ni mwaka ambao viwanda hivyo vilianza uzalishaji, shughuli kuu ya viwanda husika, idadi ya wafanyakazi waliopo, gharama za malipo mbalimbali kwa wafanyakazi, mapato yanayotokana na uzalishaj na gharama za uzalishaji.
Alisema mwaka 2013 Serikali iliamua ifanyike Sensa ya viwanda nchi nzima ili kubaini viashiria vya uchumi vitakavyosaidia kuweka mabadiliko ya muundo wa sekta ya viwanda na mchango wake katika pato la Taifa, kuboresha Sera na Programu za kukuza ajira, utekelezaji wa Malengo ya Milenia, Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025, MKUKUTA na Mpango wa Taifa wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Aidha, ameeleza kwa upande wa Dar es Salaam kazi nzuri imefanyika kwa wenye viwanda kutoa ushirikiano kwa kukamilisha ujazaji wa madodoso mafupi na marefu na tayari madodoso hayo yameshawasilishwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa uchambuzi.
Aidha, alifafanua kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara inaendelea kuhakikisha kuwa asilimia 8 iliyobaki ya viwanda vyote nchini inawasilisha taarifa husika kabla ya muda uliopangwa.
Alisisitiza kuwa kazi ya sensa iko kwa mujibu wa sheria ya takwimu ya mwaka 2012 na watakaoshindwa kutekeleza ujazaji wa madodoso hayo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Naye Kaimu Meneja Takwimu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Kapala alisema sensa hiyo ni ya kitaifa, hivyo taarifa zote zinazokusanywa ni siri na zinatumika kwa matumizi ya kitakwimu tu.
Alisema katika Sensa hiyo iliyoanza mwezi Machi mwaka huu mkoa wa Dar es salaam ulitarajia kuwa umekusanya takwimu za viwanda 1840 ifikapo Juni 8 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment